Mgahawa
aliotumia Rais John Magufuli kupata mlo wa mchana na msafara wake juzi
kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, umekuwa kivutio kwa wateja wengi
wakinunua chakula na kutaka kukalia kiti na meza alivyotumia kiongozi
huyo.
Meneja
wa mghahawa huo wa Victoria, Elizabeth Maneno (pichani) alisema jana
kwamba hali hiyo ilijitokeza mara baada ya Rais kuondoka hapo.
“Hata leo tumepokea wateja wengi kulinganisha na siku nyingine, baadhi yao wanaagiza chakula kwa sharti la kutaka kukikalia kiti na meza aliyotumia Rais Magufuli,” alisema Elizabeth.
Akizungumzia hali ilivyokuwa juzi kabla na wakati wa ugeni huo meneja huyo alisema:“Ilikuwa
ni hofu na woga uliochanganyika na furaha kumwona Rais akiingia kwenye
mgahawa wetu wa chai ya rangi ya Sh200 na ya maziwa Sh300.
“Mshtuko
wetu uligeuka furaha baada ya kubaini kuwa oda ya sahani 28 za kubeba
(takeaway), tulizoagizwa mapema asubuhi bila kuelezwa zinakoenda
zilikuwa za ujumbe wa Rais,” alisema na kuongeza:
“Kabla
Rais Magufuli hajaingia kwenye mgahawa wetu, alikuja mtu mmoja
tusiyemfahamu na kuagiza sahani 28 za chakula kwa gharama ya Sh5,000
kila moja,”
Alisema
baada ya kumtaarifu mteja wake kuwa chakula kiko tayari, alielekezwa
kuandaa meza na viti kwa sababu wageni wake (wa mteja), sasa wameamua
kula palepale mgahawani.
“Ghafla
tulimwona Rais anaingia ndani ya mghahawa wetu; kwanza tulishikwa hofu,
woga na kihoro tusijue tufanye nini hadi tulipogutushwa na aliyetoa oda
kwa kutuagiza tugawe chakula alichoagiza,” alisema meneja huyo; “hapo ndipo tulipobaini kumbe chakula kile kilikuwa cha ugeni wa Rais.”
Pamoja
na chai ya rangi na ya maziwa, mghahawa huo pia unauza vyakula vya aina
mbalimbali kwa bei kati ya Sh1,500 hadi Sh5,000 kwa vyakula vya kubeba,
huku soda ikiuzwa kwa Sh500 kwa chupa
;