Aih!
Jamani hebu tusijitoe akili huu ni mwezi wa toba mwezi wa wastaarabu
tuwaache watu wafunge siyo kujipitisha na nguo za matamanio
kuwafungulisha wenzenu mchana.Tunaendelea na kiporo chetu naona
ushakunja mdomo kwa vile nimekugusa. Dada wewee chuki nichukie lakini
yangu yachukue. Sasa tuendelee niliishia wapi vile oo nimekumbuka.
Wanawake wenzangu, kaeni mjue kwamba wanaume wana maudhi ambayo
tunatakiwa tuyavumilie, inatupasa wanawake tuwe na moyo wa chuma kuweza
kuhimili tabia za wanaume.
Siye tuliyofunzwa zamani katika mkole na msondo tuliambiwa kuwa
wanaume wana maudhi kushinda neno lenyewe maudhi, wana makusudi kuliko
makusudi yenyewe, tena ni kama watoto wadogo wanaotaka kulelewa na
hawataki kuelewa wana ujeuri wa kutaka kuabudiwa.
Nani asiyejua, jeuri ya wanaume? Jamani si kila siku tunaambiwa kuhusu unyanyasaji wao katika familia?
Mateso na manyanyaso yao yote wanawake tunatakiwa tuyavumilie wala
tusilie kwani kwa vyovyote vile siye ndiyo liwazo lao la moyo.
Hakuna mwanaume anayeweza kusimama peke yake bila ya mchango wetu!
Halo haloooo wanawake tunayo hatunayooo? Jamani usivimbishe mashavu
itikia basi... tunayooo!
Kama tunafanya kicheni pati kwa ajili ya kukusanya vyombo, basi
tusiache kufuata zile mila na desturi zetu za ndani yaani kufundwa na
makungwi na manyakanga wa enzi zile ili tupige ndege wawili kwa jiwe
moja.
Tuache kuiga mambo ya kihuni ndani ya ndoa, kwani kwetu siye ndoa ni
heshima, tunatakiwa tuilinde na tufuate masharti yake ili tuweze
kuheshimika kama mama na bibi zetu walivyoweza kula chumvi nyingi kwenye
maisha ya ndoa.
Mpo au mmelala? Haya mmelalia nini mikono au masikio? Kikubwa wanawake
wenzangu tujifunze kwa waliotutangulia, ndoa zao zilidumu kutokana na
kuwaheshimu waume zao.
Hebu waulize waliotangulia kuingia kwenye ndoa kilichowakimbiza ni
nini, lazima kwanza watajutia makosa yao kisha watakwambia kwamba siku
zote nazi haishindani na jiwe.Asikuambie mtu ndoa inataka kufuata
mafunzo siyo mwanamke kubinua midomo kwani ikikushinda utalia kila uchao
na utaongeza idadi ya wanaume na kila atakayekuoa atakuacha kwa kuwa
utakuwa umeshindikana.
Wanawake tusiwe kama kuku wa mayai waliozeeka ambao hawafai kwa nyama
kwa kukosa ladha, hebu tujiheshimu kwa mavazi na tuifuate elimu hii ili
tuzilinde ndoa zetu.
Mwari wangu usije kusema kuwa sijakwambia kwani nimeshasema sana,
angalia usichelewe kwani ukichelewa kuuanika utakuja kuutwanga mbichi,
badilika bado hujachelewa.
Ni Mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.
;