Beki wa Nigeria, William Ekong akibinuka tik tak dhidi ya mshambuliaji wa Tanzania, John Bocco katika mchezo wa leo
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
TANZANIA imejiweka njia panda katika mbio za Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Nigeria, jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taifa Stars sasa inakamilisha mechi mbili za Kundi G bila ushindi, baada ya awali kufungwa mabao 3-0 na Misri mjini Alexandria Juni mwaka huu, wakati Nigeria inafikisha pointi nne baada ya awali kushinda 2-0 dhidi ya Chad.
Kocha Charles Boniface Mkwasa aliwaanzisha wote washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, lakini hii leo waliishia kuisumbua tu ngome ya Eagles.
Mshambuliaji wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Khalfan Ngassa alifanikiwa kuwapenya mabeki wa Nigeria na kubaki na kipa Ikeme Onora lakini mara zote dakika ya 13, 22 na 58 akakosa mabao ya wazi, kabla ya kutolewa dakika ya 67 kumpisha John Raphael Bocco.
Mbwana Samatta naye dakika ya 15 aliwapangua mabeki wa Nigeria, lakini shuti lake likaenda nje.
Super Eagles walipata nafasi moja tu nzuri dakika ya 24 baada ya shuti la mpira wa adhabu wa Nahodha Ahmed Musa kupanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Tanzania, Mkwasa aliwasifu vijana wake kwa kucheza vizuri, lakini akasema bahati haikuwa yao kwani walitengeneza nafasi wakashindwa kutumia.
Kwa upande wake, Sunday Oliseh wa Nigeria alisema kipindi cha kwanza walicheza kwa kuwahofia wenyeji, na hata kipindi cha pili walipotaka kubadilika kucheza, lakini mechi ikawa ngumu.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Mudathir Yahya/Said Ndemla dk61, Mbwana Samatta, Mrisho Ngassa/John Bocco dk67 na Farid Mussa/Simon Msuva dk81.
Nigeria; Ikeme Onora, Solomon Kwambe, Kingsley Madu, Kenneth Omeruo, William Ekong, Nwankwo Obiora, Ahmed Musa, Haruna Lukman/Igboun Emeneka dk35, Emmanuel Emenike/Ujah Anthony dk61, Uzochukwu Izunna na Moses Simon/Eduok Samuel dk69.
Chanzo :binzubeiry.co.tz
;