Jayantilal Keshavji Chande ‘Sir Andy Chande’.
Imebainika kuwa, taasisi inaayodaiwa kuwa na imani yenye utata
duniani ya Freemason inaanza kupungua nguvu kufuatia wafuasi wake
kuachana na nao na kurejea kwenye imani zao za mwanzo chanzo kikiwa
kusemwa vibaya kwa taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa memba mmoja wa Freemason jijini Dar, idadi ya wafuasi
wa taasisi hiyo inapungua siku hadi siku na sasa, viongozi wake wanahaha
kutoa elimu ya kuwafanya waliobaki waendelee kubaki.
TWENDE NAYE HUYU
“Unajua wakati inaanza Taasisi ya Freemason ilipata jina kubwa sana
kwani watu wengi maarufu walijiunga, lakini sasa yale manenomaneno
kwamba kuna ibada ya kishetani, wanaojiunga wanatoa makafara ndugu zao,
mara kuna chakula cha damu, baadhi ya wanachama wakaanza kutoka kurejea
kwenye imani zao za awali,” alisema memba huyo
Pete zenye alama ya Freemason.
KUNA IBADA KWELI?
Alipoulizwa kwa nini wafuasi wamekuwa wakiondoka kwa maneno mabaya ya watu kama kweli hakuna ibada, mwanachama huyo alisema:
“Sifa mbaya, unajua wengine waliona kama wanachafuliwa lakini ukweli
wanaujua wao kwamba hakuna ibada za kishetani. Ila tunapokutana wote
tunakuwa na maneno ya pamoja kama kuashiria mshikamano wetu.”
TANZANIA KUNA WANACHAMA WANGAPI?
“Kwa Tanzania mpaka sasa kuna wanachama wasiopungua 650. Unajua kikubwa
ni masharti ya kujiunga wengi yanawabana, ndiyo maana idadi ni ndogo kwa
nchi kama hii yenye watu wasiopungua milioni arobaini.”
NI AKINA NANI?
“Wafuasi wetu wengi wanatoka katika sehemu mbalimbali, kuna walimu,
wauguzi, madaktari, watu maarufu, wafanyabiashara wakubwa na wengine ni
wanafunzi wa ngazi ya chuo. Lakini tofauti na watu wanavyosema kuwa,
kuna viongozi wakubwa wa serikali, si kweli. Viongozi wakubwa wa
serikali si wafuasi wetu ila wanaweza kutoa ushauri au kusaidia pale
inapobidi.”
KUMBE JENGO LAO LILIKUWA LA BUNGE ZAMANI
Katika mazungumzo hayo, memba huyo alisema kuwa, jengo linalotumiwa kama
Ofisi ya Freemason lililopo maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam,
lilikuwa la bunge wakati wa mkoloni na baadaye serikali ya Tanganyika
huru, mwaka 1961.
Jengo linalotumiwa na wanachama wa Freemason.
UNATAKIWA KUWA MILIONEA ILI KUJIUNGA
Tofauti na watu wanavyodai kwamba, unaweza kujiunga na Freemason ukiwa
maskini halafu ukawa tajiri, lakini mwananchama huyo alisema kuwa,
anayetaka kuwa mfuasi ni lazima aweze kutoa mchango unaofikia shilingi
milioni kuanzia kumi na kuendelea.
KAULI YA SIR ANDY CHANDE YATOA NGUVU
Maneno ya memba huyo yanashibishwa nguvu na aliyewahi kuwa kiongozi wa
Freemason ukanda wa Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande ‘Sir
Andy Chande’.
Akizungumza wakati fulani jijini Dar es Salaam kwa kuanika hali ya
Freemason nchini na duniani kwa ujumla, Sir Chandy alisema kuwa,
Tanzania ina wafuasi zaidi ya 600 ambao wanatokana na kada mbalimbali
wakiwemo watu maarufu, lakini alisema hakuna viongozi wakuu wa serikali.
HAWATAMBULIKI
Chande alisema kuwa, si kazi rahisi kumtambua mfuasi wa Freemason
lakini wao wenyewe ndiyo wanaofahamiana na kukutana katika vikao
mbalimbali ambavyo hufanyika mara moja baada ya siku thelathini.
KUHUSU IDADI KUPUNGUA
Chande alisema kuwa, awali tangu kuanzisha kwake mpaka miaka ya
karibuni, wafuasi wa Freemason walifikia 8,000,000 duniani kote lakini
kwa sasa wamefikia 6,000,000 kutokana na watu kuielewa vibaya taasisi
hiyo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel &Bible Fellowship, Zachary Kakobe.
WAFUASI WANATAKIWA KUBAKI NA IMANI ZAO
Sir Andy Chande alikwenda mbele kwa kusema kuwa, ili uwe mwanachama wa
Freemason ni lazima mtu huyo aendelee kuwa muumini wa Mungu katika imani
yake ya Kikristo au Kiislam.
UMRI NI HUU
Alisema anayetaka kujiunga awe na umri unaozidi miaka 21 na walio chini
ya umri huo hawaruhusiwi kwa sababu ya uwezo wa kutunza mambo lakini pia
akasema ili ujiunge Freemason ni lazima familia ya anayetaka kujiunga
ua ndugu zake wajue ili kuepuka matatizo utakapotakiwa kutoa michango.
UWAZI NA SHEHE MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM
Akizungumza na gazeti hili juzi kuhusu imani hiyo kuwataka wafuasi wake
wabaki kwenye imani zao, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi
Mussa Salum alisema:
“Muumini wa Kiislam, akiwa Freemason ajue si Muislam tena. Wale wana
ibada mbaya, haitokani na Mungu tunayemwamini sisi. Wewe Kama ni Muislam
halafu ni Freemason jiondoe kwenye Uislam.”
HUYU HAPA ZACHARY KAKOBE
Akizungumza na Uwazi, Jumamosi iliyopita kuhusu imani ya Freemason,
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel &Bible Fellowship, Zachary
Kakobe alisema:
“Ni unafiki mkubwa kumtumia Mungu aliyeumba mbingu na nchi halafu wakati
huohuo ukawa kwenye imani ya Freemason. Chagua moja, Mungu hataki mtu
vuguvugu. Kuwa moto au kuwa baridi ijulikane moja. Na wat wajue kwamba,
ibada yoyote nje ya Mungu wa kweli ni ushetani.”
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum.
KAMANDA SIRO NAYE ASEMA YAKE
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro yeye alisema:
“Freemason ni taasisi ipo kisheria. Ila mimi nataka kushughulika na hao
watu mnaowaandika kwamba wanajipatia pesa kwa kuuza fomu feki za
Freemason kwa njia ya utapeli. Siku moja nitavaa kiraia halafu
nitakwenda pale ofisini kwao nje nikawakamate.”
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ANENA
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Yusuf Masauni alipoulizwa juu ya
madai kuwa Freemason wanadaiwa kuwa katika imani za kishetani alisema
hayo ni madai na hawezi kuyazungumzia kwa sababu hana hakika na hicho
kinachodaiwa.