Kitaifa:Lowassa avunja mkutano Tanga


Baadhi ya wananchi wakiwa wamepoteza fahamu kutokana na msongamano kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa uliofanyika kwenye Uwanja wa Tangamano mkoani Tanga jana. 


Tanga. Mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa jana alilazimika kukatisha mkutano wake wa kampeni kabla ya muda, kwa kuhofia usalama wa wananchi waliofurika kuzidi uwezo wa Uwanja wa Tangamano mjini hapa.

Lowassa aliwasili jijini Tanga saa 10.20 jioni kwa helkopta ambayo wakati ikiwa angani ikitafuta nafasi ya kutua uwanjani hapo, Tambwe Hizza aliwaeleza wananchi kwamba kutokana na watu kuwa wengi kwenye uwanja huo, hakukuwa na mahala pa kutua, hivyo inaenda kutua uwanja wa ndege.

Msafara wa Lowassa aliyekuwa katika gari aina ya Landcruiser ya rangi nyeusi ulitokea uwanja wa ndege kwa kuongozwa na magari ya polisi, lakini hata hivyo hakuweza kufika mapema Tangamano kwa sababu watu walikusanyika kwa wingi kwenye barabara alizopita kumshangilia.

Alipofika Tangamano watu waliokuwapo uwanjani hapo kwa maelfu walianza kuminyana wakigombea kumuona huku wakimshangilia, “rais, rais, rais”.

Mara baada ya kuwasili katika jukwaa alilokuwa amepangiwa kukaa, watu walipiga kelele wakitaka apande jukwaani ili wamuone, kitendo kilichomlazimisha meneja wa kampeni wa mgombea huyo, John Mrema kumuomba awasalimie kabla ya kuketi.

Kitendo cha Lowassa kusimama na kupanda jukwaani, kilisababisha uwanja kuripuka kwa mayowe kumshangilia huku wakiimba rais, rais, rais hata alipokwenda kukaa wananchi waliendelea kuimba.

Wakati Lowassa akisalimia, msongamano wa watu uliongezeka na hivyo kusababisha wanawake kuanguka kwa kukosa pumzi jambo, lililomlazimu Mrema kuwaita wahudumu wa msalaba mwekundu kutoa msaada.

Zaidi ya watu 50 walianguka na kubebwa na polisi pamoja na wahudumu wa Msalaba Mwekundu na kupelekwa sehemu maalumu iliyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia.

Ofisa wa shirika la Msalaba Mwekundu alikaririwa akisema idadi ya watu waliozimia katika mkutano huo ilikuwa kubwa ambayo haijawahi kutoka katika mkutano mwingine mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwambeji alisema baadaye kuwa amepata faraja kwa kuwa watu wote waliokuwa wamezimia walizinduka na kurudi nyumbani salama na hakukuwa na majeruhi.

Hata hivyo baada ya mkutano huo, polisi walilazimika kupiga mabomu mawili ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wanarudi nyumbani kwa maandamano katika barabara ya Ngamiani. Akizungumzia tukio hilo RPC Mwambeji alisema walikuwa wanazuia barabara na kusababisha msongamano.

Sumaye aamua kumaliza mkutano

Wakati hali hiyo ikiendelea, Meneja wa kampeni alimkaribisha Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na alipopewa kipaza sauti alitumia dakika saba kuwatuliza wananchi waliokuwa wakisukumana kugombea kumuona Lowassa.

Sumaye aliwashukuru wakazi wa Tanga kwa kujitokeza kwa wingi na kubainisha kwamba CCM haina pa kutokea.

“CCM inatangaza kwamba Tanga ni ngome yake, hii inaashiria kwamba safari hii wana-Tanga wanahitaji mabadiliko kwa sababu umati huu mkubwa ambao sijawahi kuuona, umekuja kumshuhudia rais wa awamu ya tano,” alisema Sumaye.

Hata hivyo, Sumaye hakumaliza hotuba yake baada ya kuona watu wanaoanguka kwa kukosa hewa ikiongezeka, ndipo akasema anamkaribisha Lowassa awasalimie kisha mkutano ufungwe, watu watawanyike kwa sababu ya usalama wao.

Ahadi ya Lowassa

Aliposimama kuzungumza, Lowassa alisema alitumia muda mfupi kutoa ahadi zake kwa Wanatanga, na kubainisha kuwa kutokana na hali halisi ni wazi kwamba akizungumza zaidi watu wanaweza kufa na yeye asingependa hali hiyo itokee.

“Ninaomba nimalizie kwa kuwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi, mkutano huu unanikumbusha nilipokuwa Tanga kuomba sahihi kwenye kura za maoni za CCM..hii ni ishara kwamba mabadiliko ni lazima,” alisema.

Kabla ya kumaliza mkutano huo, Lowassa alisema akichaguliwa kuwa rais atahakikisha katika kipindi cha miezi sita bandari mpya ya Ndumi, itaanza kujengwa kwa sababu wenye uwezo wa kuijenga wapo, lakini Serikali ya CCM inawabania kwa sababu haitaki wananchi wa Tanga wainuke kiuchumi.

Mgombea huyo alisisitiza kuwa sambamba na bandari, akiingia madarakani atasimamia ujenzi wa reli ya Tanga-Arusha-Musoma hadi Kampala, Uganda kwa haraka zaidi kwa kuwa itaharakisha maendeleo.

Mgeja na ahadi za Kikwete

Kabla ya Lowassa kuwasili, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alisema mikoa ya Tanga na Shinyanga ni waathirika wakubwa wa ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete wakati akiomba urais, lakini hakuzitekeleza.

Alisema aliahidi kufufua viwanda, kujenga bandari mpya ya Ndumi na kuboresha hali ya wakulima na wavuvi, lakini hadi anamaliza muda wake hakuna hata alichotekeleza.

“Mkiona vigogo wakubwa tumeondoka CCM mjue tumekuja Ukawa kufuata mabadiliko, tumebaini ndani hakuna kitu, kule kumejaa fitina na mizengwe ya kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi, mpeni kura Lowassa na Mussa Mbarouk kwa maendeleo ya Tanga.

Kwa upande wake, Hizza alisema wagombea wa CCM wanaokwenda Tanga kuwaeleza kwamba watafufua viwanda, hawasemi ukweli kwa sababu ndiyo walioviua kwa lengo la kudhoofisha maendeleo ya wana-Tanga.

“Hapa Tanga ni kwetu, hii Tanga haikuwa hivi, wakoloni walijenga reli, bandari, miundombinu mizuri ya mawasiliano pamoja na viwanda ambavyo vilitoa ajira nyingi, lakini CCM imeviua halafu wanaahidi kuvifufua huku ni kuchezeana shere,” alisema Tambwe.

Lowassa awashangaa JK, Pinda

Akiwa Bumbuli, Lowassa ameshangazwa na Rais Jakaya Kikwete na Serikali, kushindwa kutatua mgogoro wa kiwanda cha Mponde ambao umedumu kwa muda mrefu sasa.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Soni ambao walimweleza kuwa bado wana tatizo la mgogoro wa kiwanda hicho.

“Nashangaa Rais Kikwete, waziri mkuu, mkuu wa mkoa kushindwa kutatua tatizo la kiwanda cha Mponde, hiki kitu gani! Serikali gani hii isiyokuwa na maamuzi,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Nisikilize kwa makini, nimechoka, nimechoka kusikia habari za Mponde kila siku halafu hamna suluhisho, kuna nini? Uongozi gani huu unaoshindwa kutatua matatizo madogo kama haya kwa wananchi.

“Ninawahakikishia ndani ya miezi sita nitakuwa nimemaliza suala la Mponde, uongozi wa nchi unahitaji uthubutu, fanya maamuzi hata ukikosea potelea mbali,” alisema.

Septemba 2014, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliagiza wakala wa wakulima wadogo wa chai pamoja na Bodi ya Chai nchini, kuunda timu ya watu wawili au watatu itakayosimamia mwenendo wa kiwanda hicho cha kusindika chai.

Baada ya waziri mkuu kutoa agizo hilo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiwa katika ziara za chama jimbo la Bumbuli, Septemba mwaka jana aliwaambia wananchi hao kuwa Rais Kikwete amekirejesha kiwanda hicho kwa wananchi baada ya kuwapo kwa mgogoro uliodumu kwa miaka kumi.

Hata hivyo, jana wananchi wa Bumbuli walionyesha kuwapo kwa mgogoro unaoendelea kuhusu kiwanda hicho, jambo ambalo lilimshangaza Lowassa na kuahidi akiingia madarakani Serikali yake itatatua mgogoro wa kiwanda hicho ndani ya miezi sita.

Pia Lowassa aliwaahidi wananchi hao kuwaondolea umaskini ambao umekithiri kwa kuhakikisha elimu inakuwa bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu ili wananchi wajiendeleze.

Bango la Magufuli lazua kizaazaa

Katika mkutano huo uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Kisiwani polisi waliwadhibiti vijana watatu waliokuwa wakipita pembeni ya uwanja wakiwa wamebeba bango lililoandikwa ‘Hapa Kazi Tu’.


Pia polisi iliwadhibiti wanawake wawili ambao walikuwa wakipiga kelele katikati ya uwanja huku mmoja akionekana kama amelewa, ambao waliingizwa kwenye gari la polisi na kupelekwa kituoni.

Wananchi walilizingira gari la polisi wakitaka waachiwe watu hao wawashughulikie, lakini askari walifanikiwa kuondoka nao.

Awali, mgombea ubunge wa jimbo la Bumbuli kwa tiketi ya Chadema, David Chinyegheya alidai kulikuwa na vijana wameandaliwa kuvuruga mkutano huo, hivyo aliomba polisi kuwadhibiti.

Imeandikwa na Boniface Meena, Burhan Yakub na Maimuna Msangi.

MWANANCHI


x

;

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »