Ben Pol na Avril.
MUZIKI wa Bongo Fleva kila kukicha unazidi kupaa kimataifa na hii imeleta hamasa kwa wasanii wengi kupata upenyo wa kufanya kazi nyingi kwa kushirikiana na wanamuziki wa kimataifa.Zipo kolabo za wasanii wa Bongo walizozifanya na wasanii wengine wa kimataifa kama vile KCEE na Shetta, Diamond na Davido, Diamond na Mr Flavour na nyingine kibao ambazo zimefanya vizuri.
Ali Kiba na Ne-Yo.
Kwa hivi sasa zipo kolabo nyingine za kimataifa zilizofanywa na Wabongo zinazotoka leo na nyingine zikitarajiwa kutoka mbeleni ambazo mashabiki wengi wa muziki huu wamekuwa wakizisubiria kwa hamu na katika makala haya yanaziweka wazi;
Joh Makini na Davido (Nigeria)
Davido anayebamba na Ngoma ya Dodo kutoka Albamu ya Baddest, hivi karibuni kupitia ukurasa wa Twitter alithibitisha yuko mbioni kuachia ngoma ya pamoja na rapa kutoka Bongo, Joh Makini. Mashabiki wengi wa muziki wa Hip Hop Bongo wametega masikio juu ya ujio huu ambao Joh naye amethibitisha kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Diamond na Ne-Yo (Marekani)
Prodyuza aliyepika Ngoma ya Number One, Sheddy Clever ndiye anayehusika kutengeneza kolabo hili jingine linalosubiriwa kwa hamu na mashabikindani na nje ya nchi la Diamond na Ne-Yo kutoka Marekani.
Ngoma imetengenezewa nchini Kenya ambapo Diamond amewataka mashabiki wake wakae mkao wa kuisikia hapo mbeleni.
Ben Pol na Avril (Kenya)
Leo staa wa Bongo Fleva kwa mara ya kwanza ataachia ngoma yake mpya ya Ningefanyaje ambayo amemshirikisha staa kutoka Kenya, Avril pamoja na chipukizi kutoka Bongo, Rose M.Mbali na ujio huu mashabiki pia wana hamu ya kusikia ngoma kibao za Ben Pol kama vile Sophia, Jikubali, Pete pamoja na Ningefanyaje alizofanyia kolabo na Wangechi kutoka Kenya ambazo zitaanza kusikika mapema mwezi ujao katika msimu wa tatu wa Coke Studio.
Ali Kiba na Ne-Yo (Marekani)
Ni moja ya kolabo zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki. Kupitia msimu wa tatu wa Coke Studio uliofanyika nchini Kenya, ulimualika staa wa kimataifa kutoka Marekani, Ne-Yo na kitendo hicho kilimfanya kukutana na kichwa kutoka Bongo ambacho nacho kilialikwa katika msimu huo.Kolabo hilo tayari limekamilika na kinachosubiriwa ni siku ya kuachiwa.
Young D na Patoranking (Nigeria)
Kutokana na kufanana kisura na swagga, staa wa muziki kutoka Bongo, Young D yupo mbioni kufanya kolabo na ‘pacha’ wake, Patoranking kutoka Nigeria.Young D ameshathibitisha hilo na mashabiki wametega sikio kwa hamu kumsikia katika ngoma hiyo itakayotengenezwa hivi karibuni nchini Nigeria.
;